En cours de chargement...
Elimu kuhusu utaratibu wa kufungua, kusikiliza na kusimamia mirathi na wosia Tanzania ni muhimu. Umuhimu unaongezwa na migongano katika sheria. Sheria zinaratibu aina tatu za mirathi: ya kimila, kiislamu na ya kiserikali. Sheria na taratibu kwa mfano za mirathi ya kimila au ya kiislamu inaweza kukamilisha mirathi mahakamani lakini ikapingwa kwa kutumia sheria nyingine zinazolinda haki za makundi mbalimbali.
Mapungufu haya yamechochea umuhimu wa elimu ya utaratibu wa kisheria wa mirathi na wosia kwa makundi mbalimbali Tanzania. Kitabu hiki kimebainisha sheria zinazohusiana na haki za warithi, taratibu za kupata urithi stahiki, wakfu, haki katika wosia, migongano katika sheria za kimila, kiislamu na za nchi na taratibu za mahakama zinazoweza kurekebisha mapungufu yaliyopo. Kitabu kinatoa mwanga wa namna haki za wahusika mbalimbali katika jamii zinavyolindwa na sheria mbalimbali, taratibu za kudai haki zao, vikwazo wanavyopaswa kuvitarajia, na namna ya kukabiliana na vikwazo hivyo kisheria mahakamani.
Kimejengwa kuwa msaada katika kuelezea sheria na taratibu za mirathi na pia katika kubainisha misimamo tofauti ya sheria mbalimbali kuhusu haki za mirathi kwa makundi mbalimbali. Jumla ya sheria 26, kanuni mbalimbali 11 na kesi 40 zimenukuliwa kuwezesha welewa mpana na kamili. Sehemu ya yaliyomo imebeba mada zote muhimu kumrahisishia msomaji kupata haraka kile anachokitafuta. Mazingira tata na migogoro inayojitokeza mara kwa mara vimeongezwa na kuwasilishwa kwa mpangilio sahili kuwezesha msomaji kupata mwanga wa mambo mbalimbali haraka zaidi.
Kitabu hiki ni msaada mkubwa kwa wanazuoni, wataalamu wa sheria, waheshimiwa mahakimu na majaji katika ngazi zote, na wananchi wa kawaida. Kitabu, pia, kitaongeza mwanga kwa watunga sera na watunga sheria katika maeneo yanayohitaji maboresho kwa ajili ya kujenga mfumo, sheria na taratibu kamilifu na rafiki zaidi za mirathi na wosia Tanzania.